ASSALAM ALEIKUM - ALEIKUM


Baada ya kusalimiana, Mradi wetu wa pamoja, baina ya TUKI ya Dar es Salaam na Idara ya Masomo ya Kiasia na Kiafrika ya Helsinki, Finland, umeazimia kutafiti lugha na tamaduni za Kiswahili. Lugha na tamaduni hizi za kimsingi ndizo asili pekee ya kuhifadhi mapisi na maendeleo ya lugha yetu na utamaduni asilia wa Waswahili. Katika hatua hii ya mwanzo, kunatarajiwa kupatikana data zitakazowezesha tafiti-linganifu baina ya lahaja mbalimbali na kizaliwa cha lahaja hizo yaani Kiswahili Sanifu. Ramani ya lahaja ikishachorwa na kuwekwa sawa, data za lahaja hizo na tamaduni, sanaajadiiya, fasihi n.k. zitahifadhiwa katika HIFADHI ya pamoja TUKI - Dar es Salaam na Helsinki. Makala na vitabu ni matunda yanayosubiriwa kwa hamu kubwa kuhusu kazi hii muhimu. Mabwana Arvi Hurskainen na T.S.Y. Sengo wanamshukuru sana Maalim Haji Chum kwa msaada wake wa taarifa, tajiriba masikanini na ushirikiano wake mkubwa katika kazi ya utafiti uliofanyika Wilaya ya Kusini-Unguja yeye akiwa msaidizi wa kutegemewa sana. Moja ya sifa zake kuu ni wepesi katika unukuzi; kujitolea mhanga katika ukusanyaji wa data mbalimbali na kutokuchoka katika dhamiri yake ya kuuhuisha utamaduni wa wilaya yake na hasa wa Kae penyewe.